Jinsi Kuondokana Na Tabia Ya Matumizi Mabovu Ya Fedha Na Kuweza Kujiwekea malengo


Mambo yote kuhusu fedha yanaanzia kwenye misingi miwili muhimu kuhusu fedha. Misingi hii ni mapato na matumizi. Kila kitu kuhusu fedha, iwe ni kuishiwa, kuwa masikini, kuwa tajiri na hata kuwa na akiba na kuwekeza kutaanza na misingi hiyo miwili, mapato na matumizi. Matatizo yote ya kifedha na hata mafanikio yote ya kifedha yanaanza na misingi hiyo miwili, wale wanaoweza kuisimamia vizuri wanapata mafanikio na wanaoshindwa wanaishia kuwa na changamoto za kifedha.

Karibu rafiki kwenye kipengele chetu cha USHAURI WA CHANGAMOTO mbalimbali ambazo zinatuzuia kufikia mafanikio tunayotaka kwenye maisha yetu. Kupitia kipengele hiki, wewe msomaji unaniandikia changamoto yako na mimi naijadili na kukushauri njia bora za kuondokana na changamoto hiyo. Kujua jinsi ya kutoa changamoto yako ili ushauriwe soma makala hii mpaka mwisho.

Leo katika kipengele hiki tutakwenda kujadiliana na kushauria kuhusu matumizi mabovu ya fedha ambayo yanawafanya watu kushindwa kuweka akiba na hivyo kubaki kuwa masikini. Karibu twende pamoja kwenye makala hii ya leo na mpaka kufika mwishoni utakuwa umepata mwanga wa hatua gani za kuchukua ili uweze kudhibiti matumizi yako na hatimaye kuweza kuweka akiba na hii kukufikisha kwenye uhuru wa kifedha.

Kabla hatujaingia kwenye kujadili mada ya leo, tupate maoni ya msomaji mwenzetu ambaye alituandikia kuomba ushauri juu ya changamoto hii ya kifedha;

Nikiwa na pesa mfukoni nikiona kizuri chochote na kununua bila kujali sina pesa nyingine ya akiba Na hatakama ninayo nyumbani nawaza kwenda kuichukua niwe nayo mfukoni. Naomba ushauri niondokaneje na hali hii.

Kama ambavyo tumesoma kwenye maoni ya msomaji mwenzetu hapo juu, tatizo lake ni kushindwa kudhibiti matumizi yake, badala ya yeye aiendeshe fedha, fedha imekuwa inamwendesha yeye.
Hili ni tatizo ambalo linawasumbua watu wengi, na limekuwa linawazuia wengi kufikia ndoto zao za kuwa na uhuru wa kifedha. Mtu anakuwa na mipango mizuri sana kabla hajapata fedha, ila akishazishika ile mipango yote inafutika na kujikuta anazitumia hovyo. Zikishaisha ndiyo anaanza kukumbuka kwamba alikuwa na mipango ya kifedha ambayo hajaitimiza.

Ni rahisi kuona hili kwa wengine kuliko kwetu binafsi, nenda popote na utakuta watu wakimzungumzia mtu ambaye amepata fedha nyingi kwa wakati mmoja, labda fedha za urithi au fedha za mafao, utasikia watu wakisema anatumia fedha vibaya. Lakini watu hao hao wape fedha na wataonekana wanatumia vibaya.

Fedha zimekuwa na changamoto nyingi sana kiasi ambapo zimewachanganya wengi, mpaka wengine wakaishia kuzipa majina mabaya. Na wengine wamekuwa wakiamini labda kuna nguvu zisizo za kawaida ambazo zinawaibia fedha zao. Hapa ndipo utakutana na watu wanakuambia kuna chuma ulete anawaibia fedha zao. Ukweli ni kwamba hakuna chuma ulete anayechukua fedha za mtu, bali mtu mwenyewe ndiye anakuwa chuma ulete wa fedha zake mwenyewe. Kama kungekuwa na mtu mwenye uwezo wa chuma ulete, asingehangaika na fedha ndogo ndogo za watu, badala yake angeenda kuchukua fedha nyingi benki kwa nguvu zake zisizo za kawaida.

Kama nilivyosema mwanzoni kwenye utangulizi wa makala yetu hii ya leo, changamoto zote za kifedha zinaanzia kwenye misingi miwili mikuu, mapato na matumizi.

Mapato ni ile fedha ambayo inakuja kwenye mfuko wako. Kitu chochote ambacho unafanya na watu wakakulipa ni njia yako ya kujipatia kipato. Na matumizi ni kile ambacho kinaondoka kwenye mfuko wako. Kitu chochote unachofanya kwa kutumia fedha yako ni matumizi.

Masikini wote kanuni yao iko hivi, matumizi yanakuwa makubwa kuliko mapato. Kwa njia hii wanaishi kwa madeni na hawawezi kuweka akiba yoyote. Wengi wanaishi kwa mkono kwenda kinywani, yaani chochote wanachopata wanakitumia.

Matajiri wote kanuni yao ni hii; mapato ni makubwa kuliko matumizi au matumizi ni madogo kuliko mapato. Kwa njia hii wanaweza kuweka akiba na kuwekeza, kitu ambacho kinawawezesha kupata zaidi na kufikia kwenye utajiri.

Kuna njia tatu za kutumia kanuni ya mapato na matumizi. Njia ya kwanza ni kuongeza mapato, njia ya pili ni kupunguza matumizi na njia ya tatu ni kufanya vyote kwa pamoja, kuongeza mapato na kuongeza matumizi.

Leo katika kumshauri msomaji mwenzetu tujikite kwenye kupunguza na kudhibiti matumizi. Hizo njia nyingine tutazijadili wakati mwingine.

Je unawezaje kudhibiti matumizi yako na kuweza kujiwekea akiba?
Hili ndilo swali ambalo tunahitaji kujiuliza ili kuweza kuondokana na matumizi mabaya, matumizi yanayotokana na msukumo wa hisia au mihemko. Hapa tutaangalia mambo muhimu ya kuzingatia ili kuweza kudhibiti na kupunguza matumizi ili kuweza kufikia uhuru wa kifedha.

Kwanza jua matumizi yako kwa sasa ni yapi. Unaweza kujua matumizi yako kwa kuorodhesha kila kitu unachofanya kwa kutumia fedha yako. andika kila shilingi ambayo umetumia kwenye siku saba zilizopita. Na kama huwezi kukumbuka vizuri fanya zoezi hili kwenye siku saba zijazo. Kila siku andika matumizi yako yote ambayo umeyafanya, hata kama umetumia shilingi mia tano au mia moja iandike. Usiache chochote. Wakati unafanya zoezi hili usijihukumu kwa lolote, wewe andika kila shilingi ambayo umeitumia.

Baada ya kujua matumizi yako ya kifedha, pitia orodha yako na kata yale matumizi ambayo siyo muhimu kwako. Na umuhimu upime kwa kigezo hiki, kama hutakufa kwa kukosa matumizi hayo basi siyo muhimu, yakate. Kwa njia hii kata kila matumizi ambayo kwa kuyakosa hutaharibu afya yako wala mahusiano yako na wengine. Kwa mfano sijawahi kusikia mtu kafa kwa kutokunywa soda, au kwa kutokununua nguo mpya, au kwa kutokununua gazeti. Vitu vingi vya anasa vitaondoka kwenye orodha yako hiyo.

Ukishaondoa yale matumizi ambayo siyo muhimu, sasa unabaki na orodha yako ya matumizi muhimu, haya ndiyo utakayoyafanya pekee.

Sasa hili zoezi haliishi kirahisi hivi, kuna changamoto nyingi hasa pale manunuzi yanapotokana na msukumo wa kihisia, na ili kuondokana na msukumo huu fanya yafuatayo;

1. Usitembee na kiasi kikubwa cha fedha kwa wakati wowote.
Hivyo pia usiwe na kiasi kikubwa cha fedha ambacho unaweza kukifikia kwa haraka kama vile benki au kwenye mpesa/tigo pesa. Badala yake fanya zoezi la kupata fedha kuwa gumu sana kwako, kwa mfano fungua akaunti maalumu ya benki ambayo hutaomba kuwa na kadi ya atm wala huduma za kifedha. Maana yake ukitaka fedha ni lazima uende mpaka benki, upange mstari ndiyo uchukue fedhga. Na fedha hizi zikishakua kidogo ziondoe na wekeza sehemu ambayo huwezi kuziondoa haraka.


2. Chelewesha manunuzi yako kwa muda.
Mara nyingi watu wamekuwa wakikutana na kitui na kushawishika kununua, huenda kwa mwonekano au maneno ya muuzaji. Lakini wanapofika nyumbani wanagundua kitu kile hakikuwa muhimu kwako. Hii huwatokea sana wakina dada na wakina mama hasa kwenye mavazi. Kuondokana na hali hii chelewesha manunuzi yako. Pale unapohitaji kununua kitu, jikubalie kwamba utanunua, lakini usinunue muda huo, badala yake jipe angalau siku saba za kufikiria kama kweli unataka kitu hiko. Ikiwezekana jipe hata siku 30. Ukifikiria kwa siku hizo utashangaa vitu vingi utasahau hata kama ulikuwa unataka kununua. Na hapa unahitaji kuwa na tahadhari kwa sababu wauzaji wengi ni wajanja na wanajua njia ya kukusukuma ununue muda huo, wanakuambia ni ya mwisho na hutapata tena, au bei itapanda, siyo kweli usiwasikilize, utakapohitaji utapata tu.

3. Jiwekee ukomo wa vitu unavyohitaji.
Hasa kwenye mavazi au starehe. Matumizi ya aina hii usipokuwa na ukomo utajikuta matumizi yanaongezeka kila siku. Kudhibitio hili kuwa na ukomo ambao huwezi kuuvuka. Kwa mfano kwenye mavazi jiwekee ukomo kwamba hutanunua nguo mpya mpaka uwe umeshavaa zile zote ambazo unazo kwa sasa.

4. Yatumie matumizi yako kama hamasa ya kuongeza kipato.
Njia nyingine ya kudhibiti matumizi yako ni kuyatumia kama hamasa ya kuongeza kipato chako. Na hapa unachofanya ni pale unapoona kitu ambacho unataka kununua, jiambie utanunua kitu hiko kama utaweza kutengeneza fedha za ziada, tofauti na ulizonazo sasa. Na hapa iweke akili yako kazini ili kukuonesha njia mbadala za wewe kupata fedha za kununua kile unachotaka. Kwa njia hii utaacha matumizi hayo kama hutapata kipato cha ziada, na kama utakipata basi utakuwa umejiongezea njia za kipato.

5. Kula nyumbani badala ya kula kwenye migahawa, nunua vitu vya jumla badala ya kununua kwa reja reja.
Haya pia ni mambo ambayo yanakuwezesha kupunguza gharama zako za maisha hasa pale unapokuwa na familia. Badala ya kula vyakula vya kununua, ni vyema mkapika na kula nyumbani. Na badala ya kununua vitu kwa reja reja, nunua kwa jumla, hii siyo tu inapunguza gharama, bali inakuondolea usumbufu wa matumizi madogo madogo ya kila siku.
Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kuhusu kudhibiti na kupunguza matumizi ili uweze kufikia uhuru wa kifedha.

Post a Comment

Previous Post Next Post