Mgodi wa Mwadui wasimamisha shughuli zake

Kampuni ya uchimbaji almasi ya Petra Diamonds imesimamisha shughuli zake za uchimbaji katika mgodi wake uliopo Mwadui Mkoani Shinyanga.

Hatua hiyo imekuja siku chache tu baada ya Kamati Mbili za Bunge kuwasilisha ripoti zao kwa Rais Dk. John Pombe Magufuli kufuatia uchunguzi walioufanya katika sekta ya uchimbaji madini ya Almasi na Tanzanite.

Wiki mbili zilizopita, serikali ilitangaza kukamatwa kwa vifurushi vya Almasi katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere ambavyo vilikuwa ni mali ya Petra na vilikuwa mbioni kusafirishwa kwenda Ubelgiji kuuzwa.

Maafisa wa serikali wamesema, Petra ilidanganya kuhusu kiasi na thamani ya almasi hizo ambapo, wakati kampuni ya Petra ikisema Almasi hiyo ilikuwa na thamani ya dola za kimarekani milioni 14.8, uchunguzi wa serikali ulibaini almasi hiyo ilikuwa na thamani ya dola milioni 29.5.

Hata hivyo, Petra imekanusha tuhuma hizo na kudai wako wazi katika kuripoti thamani ya Almasi yake lakini pia ni wakala wa serikali ndio unaokisia na kutoa thamani ya Almasi inayochimbwa na kampuni hiyo.

Katika waraka wake leo hii, Petra imesema pia kwamba baadhi ya maafisa wake wa ngazi za juu wanahojiwa kuhusiana na sakata hilo.

Kuhusu kufungwa kwa mgodi wake wa Williamson uliopo Mwadui, Shinyanga, Petra imesema uamuzi huo wameufikia kutokana na sababu za "kiafya na kiusalama" na kwamba wanaendelea kutoa ushirikiano kwa serikali ya Tanzania katika uchunguzi wa mkasa unaoendelea hivi sasa

Post a Comment

Previous Post Next Post