Njia sahihi ya kukabiliana na tatizo la fangasi

Wanaume wanaoishi katika maeneo yenye joto la wastani mpaka la juu ni moja kati ya kundi la watu wanaokabiliwa na maambukizi ya fangasi wa ngozi ya miguuni, kitabibu hujulikana kama ‘Tinea pedis.’

Mara nyingi ngozi ya miguuni hasa katika ngozi ngumu ya nyayo na katikati ya vidole, ndizo zinazopatwa sana na vimelea wa fangasi.

Uwapo wa unyevunyevu, joto na giza huwa ni mazalia mazuri ya fangasi wa miguuni.

Wanaume ambao wako katika hatari ya kupata fangasi za miguuni ni wale wenye dosari ya nyayo ya miguu kuwa na kiasi kikubwa cha tezi zinazotoa jasho nyayoni.

Vilevile wenye kinga dhaifu, wanaugua kisukari, wanaoishi maeneo yenye joto kali na wale wanaovaa viatu muda mwingi.

Maambukizi haya yanaweza kuwa chanzo cha kupata fangasi maeneo mengine ikiwamo katika sehemu za siri, viganja vya mikono na mwili mzima.

Uwapo wa fangasi miguuni unaweza pia kumhatarisha mwathirika kuvamiwa na bakteria rafiki wa juu ya ngozi ambao wakipenya kwa ndani ya ngozi huleta madhara.

Vimelea wa fangasi ni mojawapo wa vimelea wanaoweza kusambaa na kumpata mwanadamu mmoja kwenda kwa mwingine kwa kugusana na vitu vilivyotumiwa na mwenye vimelea wa fangasi.

Katika maisha ya kila siku mara nyingine watu huweza kuvaliana soksi na viatu; hii ni mojawapo ya njia zinazoweza kueneza maambukizi ya fangasi wa miguuni kwa wanaoishi mazingira ya pamoja.

Si hivyo tu bali pia kuvaa viatu na soksi za mitumba ambavyo pengine vimetumiwa na mtu mwenye maambukizi ya fangasi, inaweza pia kuwa sababu mojawapo ya maambukizi ya fangasi za miguuni.

Vilevile kutumia pamoja sakafuni au vitu vilivyokanyagwa ikiwamo mazulia, mabwawa ya kuogelea, vifaa vya mazoezi vilivyotumiwa na mtu mwenye vimelea.

Dalili kubwa ya fangasi ni muwasho unaokulazimisha kujikuna na kujihisi raha au utulivu unapojikuna, harufu nzito ya kuoza katika miguu, kumomonyoka ama kulika kwa ngozi yenye fangasi.

Pia kuvuja kwa majimaji yenye kuteleza na harufu nzito, maumivu au kuhisi kuchomachoma baada ya kuchubuka na pia mara nyingine kuhisi kuwaka moto.

Ugunduzi wa fangasi wa ngozi ya miguu ni rahisi, huhitajiki kwenda maabara, wahudumu wa afya wanaweza kugundua kwa kupata historia ya dalili na kutazama kwa macho.

Mara nyingine unaweza usihitaji kupewa dawa za kukabiliana na fangasi wa miguu, elimu ya afya inaweza kukubadili tabia na ukadhibiti fangasi wa ngozi ya miguuni bila dawa.

Njia ya kukabili fangasi
Moja ya njia rahisi za kukabiliana na kujikinga na fangasi ni kubadili mienendo ya kimaisha ikiwamo kupenda kuwa msafi wa kimwili pamoja na kufua nguo zinazovaliwa ikiwamo soksi ambazo wengine huzivaa kwa muda mrefu bila kuzifua. Tumia soksi zenye asilimia nyingi ya pamba ili kuweza kunyonya jasho la miguuni, kutumia kitambaa safi au taulo dogo kwa ajili ya kukaushia maji baada ya kuoga au unapotoka kazini, matembezini na mchezoni.

Mara tu baada ya kutoka katika shughuli zako vua viatu vya kufunika na tumia viatu vya wazi, kausha kwa kitambaa kikavu maeneo ya miguuni katika upenyo wa vidoleni.

Matibabu ya dawa za fangasi za kupaka zilizo katika mtindo wa poda zinaweza kutumika kutibu, kwa fangasi sugu, dawa za kumeza zinaweza kutolewa. Kama kukiwa na maambukizi mchanganyiko na bakteria dawa za antibiotic zinaweza kutolewa.

Mara nyingine fangasi zinaweza kupata nyufa za vidoleni zikatengeneza vidonda ambavyo vinaweza kupata maambukizi wa bakteria ikiwamo wale wa tetenasi.

Hakikisha pia ukiwa una tatizo hili kiasi cha kufikia kupata vidonda miguuni, hakikisha unapata chanjo ya tetenasi kama hukuwahi kuchomwa.

Fangasi za miguuni ni ugonjwa kama magonjwa mengine, hivyo wanaogua wasipuuze wakidhani ni tatizo dogo.

Wanaogua tatizo wafike katika huduma za afya mapema kwa ajili ya ushauri na matibabu

Post a Comment

Previous Post Next Post