Baraka zawashukia wakulima wa mbaazi masoko matatu ya nje ya nchi yamepatikana

Neema Yawashukia Wakulima wa Mbaazi Masoko Matatu ya Nje Yapatikana


 
Baada ya kukosa soko la uhakika kwa miezi mitatu huku wakulima vijijini wakilazimika kuuza mbaazi zao kati ya Sh150 na 200 kwa kilo, hatimaye masoko matatu yamepatikana nje ya nchi.

Masoko hayo yametajwa kuwa katika nchi za Dubai, Afrika Kusini na Uingereza. Katika baadhi ya maeneo ya vijijini ikiwamo mkoani Lindi, wakulima wa mbaazi wanauza hadi Sh150 kwa kilo.

Kudorora kwa soko la mbaazi nchini kulitokana na baadhi ya nchi ikiwamo India kuzuia uingizwaji wa zao hilo kutoka Tanzania.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Quality Pulse Exporters, George Fererra alisema jana kuwa, kuanzia sasa wameanza kufungasha mbaazi baada ya kupata masoko hayo.

Kampuni hiyo ambayo ipo katika Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji (EPZA), ililazimika kusitisha ununuzi na ufungashaji wa zao hilo, huku mzigo wenye thamani ya Dola 500,000 za Marekani (sawa na zaidi ya Sh1 bilioni) ukikosa soko.

Ferrera alisema uamuzi wa India kusitisha ununuzi wa mbaazi kutoka Tanzania umewaathiri wakulima na wafanyabiashara kutokana na kuporomoka bei kwa kuwa zilikuwa zikiuzwa kwa wingi nchini humo.

“Kampuni nyingi za Tanzania zilitegemea soko la India pekee na hatukuangalia sehemu nyingine. Hili ndilo kosa kubwa tulilolifanya,” alisema.

Mkurugenzi wa Mipango na Maendeleo wa EPZA, Lamau Mpolo alisema ili kukabiliana na ushindani wa soko ni muhimu kwa viwanda kuongeza tija kwenye uzalishaji

Post a Comment

Previous Post Next Post