NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamadi Masauni, amemwagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Meja Jenerali Projest Rwegasira kuunda tume kuchunguza Sh milioni 70 zilizotolewa na Serikali kujenga vyoo katika Gereza la Isanga mkoani hapa.
Pia amepiga marufuku ujenzi wa nyumba katika eneo la gereza hilo.
Akizungumza jana akiwa gerezani hapo, Masauni alisema kuna taarifa ya kuwapo ubadhirifu wa Sh milioni 70 zilizotolewa na Serikali kwa ujenzi wa vyoo vya 32 katika gereza hilo.
“Kwamba inasemekana kuna ubadhirifu wa fedha zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa vyoo vya Magereza ya Isanga.
“Namwagiza Katibu Mkuu kuunda tume ifanye uchunguzi tuweze kupata majibu na kuchukua hatua stahiki kwa wale watakaobainika kuhusika,” alisema.
Masauni alishangaa mradi huo kuchukua zaidi ya miaka mitatu na kuhoji ni kwa nini umechukua muda mrefu kukamilika.
Naibu Waziri pia amepiga marufuku ujenzi wa nyumba katika eneo la gereza hilo hadi uchunguzi utakapokamilika ni nani mmiliki halali wa eneo hilo.
Inadaiwa baadhi ya watu wakiwamo watendaji wa iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) walijigaia viwanja na kujenga katika eneo hilo la gereza.
“Kipindi hiki wakati haya maelekezo yanafanyika ni marufuku kwa mtu yeyote kuendeleza ujenzi katika eneo hili awe na kibali, awe hana, kiwe cha kweli au cha uongo, hili ni jeshi.
“Nimeishaagiza askari magereza wamshughulikie yeyote ambaye atakuja kufanya shughuli za ujenzi katika eneo hili kabla jambo hili halijapatiwa ufumbuzi wa kudumu,” alisema
Post a Comment