Rais Magufuli atishia kuifuta Benki ya Walimu



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amesema kuwa mwelekeo wa benki ya Walimu hauridhishi na inawezekana ikafutwa na kufilisika kabisa.

Rais Magufuli ameyasema hayo leo katika hotuba yake wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT)  na kuongeza kuwa kati ya benki 58 zilizopo nchini, benki ya wlimu ni miongoni mwa ambazo zina muelekeo wa kufutwa.

“Nilialikwa kwenda kufungua benki ya walimu sijaenda kufungua. Nilitamani kwenda kuifungua lakini nilipopewa ripoti na BoT nilisikitika. Tuna benki sasa hivi katika nchi hii benki 58, lakini benki ambazo zina mwelekeo wa kufutwa na kufilisika na ninyi mmeweka mtaji wenu mojawapo ni benki ya walimu,” amesema Rais Magufuli.

Rais aliwataka walimu kuhoji namna ambavyo fedha walizoziwekeza zinavyotumika katika kuendeleza benki hiyo na maslahi ya walimu.

“Sitaki kuwaficha walimu wenzangu. Ni lazima muulize hiyo mitaji mliyoiweka pale imeenda wapi. Mliowaweka pale wana maslahi ya walimu?,” amehoji Rais Magufuli.

Aidha rais magufuli amewahakikishia walimu wote wanaodai madeni yao kwa serikali kuwa watalipwa mara baada ya uhakiki kukamilika endapo tu madeni yote ni halali.

“Nataka kuwaahidi kwamba haya madeni ya walimu, hata kama yangekuwa bilioni ngapi, Kama ni madeni halali nawahakikishia kuwa nitayalipa yote. Nataka niwaahidi walimu wenzangu, mara baada ya kazi hii ya uhakiki kumalizika, wale wote wanaodai madeni halali watalipwa,” alisema Rais Magufuli

Post a Comment

Previous Post Next Post