Wamachinga wapewa siku tatu kuondoka Kwa hiari eneo la ubungo

Wamachinga wa Ubungo Wapewa Siku 3 Kuondoka
WAFANYABISHARA wadogo wadogo, maarufu kama wamachinga, zaidi ya 2,000 walio katika makutano ya barabara za Morogoro, Sam Nujoma na Mandela katika eneo la Ubungo Mataa, Manispaa ya Ubungo jijini Dar es Salaam-

Wamepewa siku tatu kuondoka katika maeneo hayo kwa hiari, ili kupisha ujenzi wa mradi wa barabara za juu (fly over).

Baada ya amri hiyo, wamachinga hao waliridhia kuhamia katika soko la Mawasiliano, ambalo limetengwa na Manispaa ya Ubungo kwa ajili yao, baada ya kufanya mazungumzo na Meya wa Manispaa hiyo, Boniface Jacob.

"Tunawapa siku tatu, leo (jana) endeleeni na shughuli zenu hadi Jumamosi mchana muanze kuondoka," alisema Meya Jacob. "Atakayekutwa hapa Jumapili, mimi simo."

Alisema aliamua kufanya mazungumzo na wamachinga hao, ili kuwapatia suluhisho la wapi pa kwenda kufanya biashara zao badala ya kuwaacha na maswali.

Aidha, Meya Jacob alisema wametenga eneo lenye ukubwa wa hekari 12 katika kituo cha Mawasiliano, ambacho ni moja ya vituo vikubwa vya daladala, ambalo litatosha wafanyabiashara 5,000.

"Wamachinga mlioko kando ya barabara eneo hili la Ubungo ni 2,000," aliwaambia meya huyo. "Mawasiliano kuna eneo la kutosha la wafanyabiashara 5,000."

"Hivyo nawasihi kuhamia kule na kama atakuwapo atakayelazimisha kubaki hapa ahakikishe anakaa nje ya mipaka iliyoweka kwa ajili ya kazi hii au kwenda eneo lolote ndani ya jiji la Dar es Salaam."

Jiwe la msingi la mradi huo liliwekwa na Rais John Magufuli mahala hapo Machi 20, mwaka huu.

Rais Magufuli, katika hotuba yake ya uzinduzi, alitaka ujenzi ukamilike kabla ya miaka miwili na nusu ya ratiba ya ujenzi.

BILIONI 186.8/-
Jacob pia alisema vijana wenye ujuzi mbalimbali watapata ajira katika mradi wa flyover na kwamba mama lishe ameshawapatia fursa ya kuwauzia chakula wafanyakazi na vibarua zaidi ya 5,000 watakaohusika na mradi huo.

Mradi wa flyover Ubungo utajengwa na mkandarasi kampuni ya China ya CCECC kwa Sh. bilioni 188.7, ambapo kati ya hizo, Benki ya Dunia (WB) imetoa Sh. bilioni 186.8 na serikali Sh. bilioni 1.9 za usanifu mradi.

Naye Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, John Kayombo, alisema mradi huo unatarajiwa kuanza muda wowote. Alionyesha mipaka, kuzungumza na wafanyabiashara hao pamoja na kuwapa muda wa kuondoka eneo hilo.

Mfanyabiashara katika eneo hilo la Ubungo Mataa, Jumanne Nasoro, alisema hawana budi kupisha eneo hilo kwa sababu wasipopisha wanaweza kuharibiwa mali zao.

Pia aliiomba serikali kukarabati na kuweka miundombinu imara katika masoko wanayopangiwa kuhamia, ili kuondokana na changamoto ya wateja kutokuingia humo kwa sababu mbalimbali.

Wakati huo huo, Meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob amesema wameanza ukarabati wa soko na eneo la Mawasiliano kwa ajili ya kurahisisha kuingia na kutoka ndani ya soko hilo.

"Kuna mpango pia wa kupitisha barabara ya mwendo kasi kwa ajili ya kushusha abiria katika kituo cha Mawasiliano hali ambayo itasaidia kuboresha biashara katika soko letu katika siku za usoni," alisema Jacob.
 

Post a Comment

أحدث أقدم