Chanzo cha Freeman mbowe kunyanga'nywa gari


Hiki Hapa Kisa cha Mbowe Kunyang'anywa Gari Bunge Lafafanua


OFISI ya Bunge imesema Kiongozi wa Kambi ya Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe hajanyang’anywa gari.

Taarifa iliyotolewa na Bunge leo Alhamisi imesema kilichotokea ni kwamba, gari hilo limerudishwa nchini ili dereva afuate utaratibu wa kupata kibali cha kusafiri nje ya nchi.
Mbowe yuko Nairobi nchini Kenya ambako Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu anaendelea na matibabu baada ya kushambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi Septemba 7 akiwa nyumbani kwake Area D mjini Dodoma.

Bunge limesema ni kweli gari lenye namba ya usajili STL 4587 aina ya Toyota Prado limetengwa maalumu kwa ajili ya kumuhudumia Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika kutekeleza majukumu yake ya kikazi na binafsi nchini.

“Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni aliomba gari ikamhudumie mjini Nairobi nchini Kenya na Ofisi ya Bunge iliridhia ombi hilo na kuomba taratibu zizingatiwe. Hata hivyo, ofisi iligundua kwamba gari ilikwenda Nairobi na dereva hakupata kibali cha kusafiri nje ya nchi ambacho kila mtumishi wa umma anayesafiri nje ya nchi lazima apate kibali hicho kutoka kwa Katibu Mkuu Kiongozi,” imesema taarifa ya Bunge.

Bunge katika taarifa hiyo limesema kwa kuwa utaratibu haukukamilika, dereva aliambiwa alirejeshe gari hilo nchini na kuliegesha katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha hadi utaratibu mwingine utakapokamilika.

“Dereva yupo Dodoma anakamilisha taratibu ili ofisi iweze kumuombea kibali Ikulu ndipo anaweza kurejea nchini Kenya kwa ajili ya kuendelea kumhudumia Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni,” imesema taarifa.

Ofisi ya Bunge imesema inasikitishwa kutokana na utaratibu unaotumiwa na Ofisi ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni wa kuzungumzia masuala yanayohusu ofisi hiyo kupitia kwa msemaji wa chama kama inavyoonekana kwenye mitandao ya kijamii akitoa malalamiko kwa niaba ya ofisi hiyo.

“Ni vyema ikaeleweka kwamba Ofisi ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ni kama ofisi nyingine zinazohudumiwa na Sekretarieti ya Bunge ambayo inapaswa kufuata kanuni na taratibu za uendeshaji wa Ofisi na ni kosa kwa mtumishi kwenda kinyume na masharti ya Utumishi wa Umma,” taarifa hiyo imesema.

Imeelezwa katika taarifa kuwa ni dhamira ya Ofisi ya Bunge kuendelea kumhudumia Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa kufuata misingi na kanuni za utumishi wa umma na zile za Bunge bila kuchanganya na siasa.

“Ofisi ya Bunge inauhakikishia umma kuwa taratibu zikishakamilika Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ataendelea kuhudumiwa popote atakapokuwa,” imesema taarifa hiyo. 

Post a Comment

أحدث أقدم