Ajiua kikatili


MWALIMU wa Shule ya Sekondari Mtenga iliyopo Kata ya Mtenga Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa, Leonard Mwipugi (29) amejiua kwa kujikata mwenyewe koromeo lake kwa kisu cha makali ya pande mbili.

Mwalimu huyo mwenyeji wa Mkoa wa Iringa, alizaliwa mwaka 1988 na alianza kufundisha shuleni hapo mwaka 2014. Ameacha mke na watoto watatu, wa mwisho akiwa na umri wa wiki mbili.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, George Kyando amethibitisha kutokea kwa tukio hilo jana saa sita mchana katika kijiji cha Mtenga wilayani Nkasi ambapo Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.

Aliongeza kuwa mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha maiti kwenye Hospitali Teule (DDH) mjini Namanyere huku mwajiri wake akifanya taratibu za kuusafirisha mwili wake kwenda kwao kwa maziko.

Mratibu Elimu Kata ya Mtenga, Hebron Mwafungo alilieleza gazeti hili kwa njia ya simu kutoka eneo la tukio kwamba mwalimu huyo aliacha ujumbe wa maandishi ukieleza kuwa mtu yeyote asilaumiwe wala kuhojiwa juu ya kifo chake.

Aliongeza kuwa ni wiki tatu zimepita tangu mwalimu alipoenda kumchukua mkewe mkoani Iringa ambako alienda kujifungua na kwamba siku hiyo ya tukio mkewe akiwa na mwanawe mchanga walikuwa wamekwenda mjini Namanyere.

Akisimulia mkasa huo Diwani wa Kata ya Mtenga, Pancras Malyatabu alisema kwa njia ya simu kuwa Mwipugi alikwenda shuleni kama kawaida hadi saa nne asubuhi alipotoka kwa ajili ya kwenda kunywa chai nyumbani kwake, kwanza alipitia sokoni kununua nyama.

“Alipofika nyumbani kwake alimuuliza mdogo wake alipo shemeji yake … alielezwa kuwa amekwenda mjini Namanyere ….. basi akamwagiza mdogo wake huyo aende kusaga mahindi huku yeye akiendelea kukatakata nyama aliyoinunua sokoni kwa ajili ya kitoweo.”

Aliongeza kuwa mdogo wa marehemu aliporejea nyumbani aliendelea na shughuli zake ndipo baadaye mgeni ambaye ni mke wa Mkuu wa Shule ya Sekondari Mtenga alifika nyumbani hapo akiwa na kikapu kilichokuwa na zawadi kwa ajili ya mama mzazi ambaye ni mke wa marehemu ambaye alikuwa amejifungua wiki mbili zilizopita.

“Mdogo wa marehemu alipopokea kikapu hicho na kwenda kukiweka chumbani kwa kaka yake ndipo aliposhituka kumuona kaka yake akiwa amelala kitandani huku nguo zake zikiwa zimelowa damu,” alisema

Post a Comment

أحدث أقدم