Ewura yawapa ushauri jamii kuwatumia mafundi umeme wenye leseni

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) ni Taasisi ya Udhibiti wa huduma za sekta mtambuka iliyoundwa kwa Sheria EWURA, Sura ya 414 ya Sheria za Tanzania.

Shughuli kuu za Mamlaka ni pamoja na kudhibiti sekta za Nishati na Maji Tanzania Bara. EWURA ina wajibu wa kuzidhibiti sekta hizi kiufundi na kiuchumi. Sekta ndogo zinazothibitiwa na Mamlaka ni Petroli, Gesi Asilia, Umeme na Maji na Usafi wa Mazingira.

Moja ya majukumu makuu ya EWURA ni kutoa, kudurusu na kufuta eseni za huduma mbalimbali inazozidhibiti ikiwemo leseni za Makandari wa Umeme na wote wanaojihusisha na shughuli za utandazi na ufungaji umeme kwa ngazi/ madaraja mbalimbali.
Mfano wa leseni ya kufunga umeme iliyotolewa na EWURA

Kwa mujibu wa kifungu cha 8(1) cha Sheria ya Umeme ya mwaka 2008, kazi za ufungaji umeme ni shughuli inayohitaji leseni ya EWURA. Kwa mantiki hiyo, ni kosa la jinai kuendesha shughuli za ufungaji umeme bila kuwa na leseni halali iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).

Hivyo basi, mtu yeyote atakayepatikana na hatia ya kuendesha shughuli hizo bila leseni, atatozwa faini ya shilingi za Kitanzania milioni tano, au kifungo cha miaka mitano au adhabu zote kwa pamoja.

Katika utekelezaji wa jukumu hili, Mamlaka imebaini kupitia kaguzi mbalimbali zinazofanywa mara kwa mara, kuwepo kwa mafundi wengi wasio na leseni za EWURA, na wengine wanaendelea kutumia leseni mfu zilizokuwa zikitolewa na Wizara ya Nishati na Madini, ambazo hawajazihuisha hadi leo.

Aidha imebainika pia kuwa, upo udanganyifu unaofanyika kati ya wenye leseni na wasio na leseni kwa kuwagongea mihuri kazi zao au kushirikiana na wafanyakazi wa TANESCO wasio waaminifu, hata kama inaonekana dhahiri kuna udanganyifu katika nyaraka husika. Kwa mantiki hiyo, wito unatolewa kwa watanzania kuwa na desturi ya kutumia mafundi umeme waliosajiliwa na wenye leseni halali zilizotolewa na EWURA ili kuhakikisha usalama wao pamoja na wa mali zao; ikizingatiwa kuwa wapo mafundi umeme wengi hapa nchini wasiosajiliwa na wanaofanya kazi za umeme bila usimamizi, na wengine ni vishoka; hivyo kazi nyingi zinafanywa chini ya viwango, na pengine kuweza kutokea ajali za moto muda mfupi tu baada ya kutumia huduma zilizotolewa na mafundi hao.

Ni muhimu wanachi kutambua kuwa wanapaswa kutumia mafundi wenye leseni kufanya shughuli za kufunga umeme katika makazi na nyumba zao ili kuweza kupunguza madhara, ajali au majanga ya moto yatokanayo na umeme; kuweza kupata fidia stahili ya bima inapotokea ajali ya moto uliosababishwa na umeme; kujiridhisha kuwa mafundi na/au kampuni za kusambaza umeme katika eneo husika zinazingatia viwango vya ubora vilivyothibitishwa na TBS na kuwa wanaofanya kazi kwa mujibu wa Sheria na kanuni za ufungaji umeme.

Kwa kutumia mafundi umeme wenye leseni, ni rahisi kufanya ufuatiliaji wa aliyefungia umeme katika makazi endapo kutatokea tatizo lolote kutokana na huduma iliyotolewa; na ni njia ya kushirikiana na Serikali katika kupiga vita mafundi umeme wanaofanya kazi bila kua na leseni wala kufuata taratibu wanaotambulika maarufu kwa jina la “VISHOKA” ambao wamekua wakiwarubuni watu bila kujua.

Vilevile, ni jambo jema kujihusisha na mtu anayetambuliwa na Serikali kuliko yule asiyefahamika vyema kuhusu uwezo wake katika kuendesha shughuli za ufungaji umeme; na ni rahisi kupata mtaalam sahihi mwenye leseni yenye daraja sawia na ukubwa na aina ya kazi inayotakiwa kufanywa; ikiwemo kugundua hatari inayoweza kujitokeza mbeleni katika mfumo wako wa umeme kabla haujaleta madhara na hatimaye kushugulikiwa mapema ili kuimarisha usalama wa watu pamoja na mali.

Kiuchumi, hupunguza gharama ya kazi kwa kutumia mafundi waliosajiliwa kwa kuwa gharama za vifaa vitakavyotumika kufunga umeme vitakadiriwa kwa usahihi na ni rahisi kupata mtaalam sahihi mwenye leseni yenye daraja sawia na aina ya kazi itakayofanywa.

Zipo athari nyingi zinazoweza kujitokeza kutokana na kuendelea kutumia mafundi umeme wasiosajiliwa na wasio na leseni ambazo ni pamoja na matumizi ya vifaa visivyokidhi viwango ambavyo mara nyingi husababisha ajali za moto; na fundi asiye na elimu na ujuzi stahiki hawezi kutambua kwa urahisi, hivyo kupelekea athari kubwa.

Vilevile kwa sababu ya kupunguza gharama fundi asiye na ujuzi stahiki hutumia vifaa visivyokidhi kwa kuwa labda bei yake ni ndogo na hali inazidi kuwa mbaya kwa aliyefungiwa umeme.

Athari nyingine ni kutokuwa na mfumo mzuri wa kuweka kumbukumbu kupitia usajili/Udhibiti, hatimaye mafundi hawawajibiki inapotokea ajali inayosadikiwa kutokana na umeme, kwani ni vigumu kuwapata kwa kua aidha hawana ajira ya kudumu au mahali (ofisi) pa kudumu.

Pia, kutumia mafundi wasiosajiliwa husababish kukosekana kwa utaratibu wa kukagua miundombinu ya umeme katika majengo yetu; hatimaye ajali kutokea baada ya miaka mingi kutokana na uchakavu wa mifumo ya umeme.

Vilevile kumekua na kasumba ya kulituhumu sShirika la Umeme nchini TANESCO pale inapotokea moto uliotokana na hitilafu ya umeme ingawa inawezekana siyo chanzo cha moto huo, kwani tatizo la umeme (electric fault) inaweza kutokana na tatizo la kiufundi, matumizi ya vifaa visivyo na ubora na matumizi yasiyofaa ya umeme.

Ili kuleta nidhamu katika tasnia ya utandazaji wa mifumo ya umeme, Mamlaka inawataka mafundi wote wa umeme kuwa na leseni zinazotolewa na EWURA, ambazo zimeboreshwa kulingana na mazingira ya sasa ya teknolojia.

Aidha, Makampuni ya umeme yanatakiwa kuajiri mafundi wenye leseni au kuwasaidia mafundi wao kuwa na leseni, siyo kuwa na leseni moja tu kwa Msimamizi halafu wengine wote wasiwe nayo, ili tu waendelee kufanya kazi kwao; kwa kuwa siyo rahisi msimamizi kufuatilia ubora wa kazi katika hatua zote za utandazi wa umeme, maana nyaya huwa zimefunikwa na mabomba au udongo au insulation, na athari za kazi mbaya zinaweza kutokea miaka kadhaa baada ya kazi kufanyika.

Vilevile, Makampuni yanayotoa huduma za utandazi wa umeme yanapaswa kuwaendeleza kiujuzi wafanyakazi mahala pa kazi na kuwasaidia wanapohitaji kusoma ili kupata daraja za juu zaidi za utaalam ikiwa ni pamoja na kuhakiki vyeti vya wafanyakazi wao kwani imebainika kuwa baadhi ya waombaji wa leseni hutumia vyeti vilivyogushiwa vya elimu ya ufundi (VETA), jambo ambalo ni kosa la jinai kutumia nyaraka zisizo halali.

Ni vyema pia vyuo vilivyoenea maeneo mengi nchini vitoe elimu ya viwango vinayokubalika katika soko, hasa katika kipindi hiki ambacho kuna ongezeko kubwa la majengo ya makazi, biashara na viwanda. Na kwa upande wa mafundi wasiopata ajira za kudumu wajiunge katika vikundi vinavyotambulika kisheria ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi bila kuvunja sheria.

Njia bora ya udhibiti ni kwa kujidhibiti mwenyewe, hivyo kwa yeyote anayehitaji kupata huduma za kufungiwa umeme katika makazi yake yampasa kutumia mafundi wenye leseni ili aweze kuepuka hatari nyingi na madhara yanayoambatana na mifumo ya umeme isiyo salama.

Ili kutekeleza majukumu na wajibu wake kwa uwazi na katika namna yenye manufaa kwa wote, EWURA inafuata sera za Kisekta, Sheria kuu na miongozo na kanuni mbalimbali zinazotolewa na Mamlaka. Sera na Sheria zinazosimamia utekelezaji wa majukumu ya EWURA ni pamoja na: Sera ya Taifa ya Nishati (2015), Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (2001), Sheria ya Umeme (2008), Sheria ya Petroli (2015), Sheria ya DAWASA sura ya 273, Sheria ya Maji safi na Usafi wa Mazingira (2009); pamoja na miongozo na kanuni mbalimbali zilizondaliwa na Mamlaka katika kusimamia utekelezaji wa majukumu yake.

Nyingine ni Sheria zinazoanzisha Taasisi ambazo zinasimamia na kuratibu utoaji wa huduma kwa kuzingatia viwango vilivyowekwa ambazo ni Mamlaka ya Usimamizi wa Usalama mahali pa kazi (OSHA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC).

Post a Comment

أحدث أقدم