Jafo anena mazito Kwa shule za serikali


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi, Selemani Jafo ameagiza wanafunzi wa shule za Serikali kufanya mtihani wa mchujo kabla ya kupandishwa vidato.

Pia, amesema hatapanga ada elekezi kwa shule binafsi bali watapunguza wenyewe.

Jafo ametoa kauli hiyo Jumatano mjini Dodoma alipozungumza na wafanyakazi wa Tamisemi.

Ametoa kauli hiyo akisema shule kongwe za Serikali zimekuwa ‘zikikimbizwa’ na za binafsi.

"Naagiza kuanzia leo, lazima wanafunzi wa shule za Serikali wafanye mitihani mara mbili, mwezi wa sita na mwisho wa mwaka ili kuwachuja wa shule zenye vipaji maalumu na kuwarudisha shule za kawaida za Serikali, vinginevyo ndiyo maana tunafanya vibaya wakati wote," amesema.

Amesema katika mchujo huo, wanafunzi watatolewa kutoka shule kongwe na kupelekwa za vipaji maalumu na vivyo hivyo kutoka vipaji maalumu kwenda shule kongwe.

Kuhusu ada kwa shule binafsi amesema si jukumu la Serikali bali wanataka kuboresha shule zake ili watu na taasisi binafsi zikose wanafunzi.

"Mheshimiwa Kakunda (Joseph –Naibu Waziri Tamisemi) nakuagiza kuanzia leo maana wewe ndiyo nimekukabidhi jukumu la elimu, nataka mtihani wa 2019 shule za vipaji zote 22 ziongoze mtihani wa Taifa na shule binafsi ziwe nyuma, lakini tuongoze kwa halali si ubabaishaji hapo ndipo shule binafsi za makanjanja zitajifuta zenyewe," aliagiza Jafo.

Wakati huohuo, Jafo amewaagiza watendaji katika idara ya elimu kushughulika na wakuu wa shule kongwe zote ili kuona kama bado wana sifa za kuendelea kuwa wakuu wa shule au kuwaondoa wanaoonekana kushindwa kazi.

Kuhusu watendaji wa Tamisemi amesema hataki mambo matatu wizarani hapo ambayo ni ulegevu, mazoea na kutojali muda ambayo amesema ni adui wa mafanikio.

Naibu waziri, Kakunda amesema hana shaka na kazi aliyopewa akiahidi kuifanya kwa kutumia weledi na uzoefu wake ili kuibadilisha Tamisemi.

Kakunda ambaye kabla ya kuwa mbunge alikuwa mkurugenzi Wizara ya Maji amesema mipango mingi anaijua lakini akaomba ushirikiano kwa watumishi.

Post a Comment

أحدث أقدم