Mwanamama aongoza kuokoa uhai wa Lissu

Jumla ya dola za Marekani 29,320 (Sh. milioni 64.447) zimechangwa na watu wa nje ya nchi kusaidia matibabu ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) huku Yasinta Massawe akiongoza kwa kutoa mchango mkubwa zaidi.

Lissu ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria (TLS) na Mwanasheria Mkuu wa Chadema, anaendelea na matibabu katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum (ICU) cha Hospitali ya Nairobi, Kenya alikolazwa tangu usiku wa Septemba 7.

Mtaalamu huyo wa sheria alilazimika kutolewa katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Dodoma na kuwahishwa kwa ndege kwenda Kenya, ili kupata matibabu ya kibingwa zaidi kutokana na kupigwa risasi na watu wasiojulikana mjini Dodoma.

Kwa mujibu wa mtandao wa kompyuta wa www.gofundme.com/Lissumedicalcare, hadi jana saa 6:44 mchana, watu 644 walio nje ya mipaka ya nchi walikuwa wamechangia dola za Marekani 29,320 kupitia kampeni maalum ya kusaidia matibabu ya mbunge huyo iliyoanzishwa na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vincent Mashinji Septemba 12.

Kwa mujibu wa orodha hiyo ya michago katika mtandao huo, Yasinta ndiye aliyetoa kiwango kikubwa cha fedha kusaidia matibabu ya mbunge huyo. Mtandao huo unaonyesha mwanamke huyo alitoa mchango wa dola 3,000 (Sh. milioni 6.594) siku 21 zilizopita.

Baadhi ya wachangiaji wengine ni Alexis Bisangwa aliyetoa dola za Marekani 500, Stanley Lucas dola 400, Kelvin Assey dola 300, familia ya Ulimwengu, Lee Kane, Khadija Jaffar, Amelda Minja, Shuu Hababa na Richard Mollel ambao kila mmoja amechangia dola 200.

Wakati wadau mbalimbali wakiendelea kujitokeza kusaidia matibabu ya Lissu, familia ya mbunge huyo ilieleza wiki iliyopita kuwa imeingia makubaliano na uongozi wa Bunge kushughulikia matibabu yake. Hata hivyo, ilielezwa kuwa makubaliano hayo ni siri kati ya pande hizo mbili.

Lissu alishambuliwa kwa risasi 32 nje ya nyumba yake mjini Dodoma majira ya mchana na watu wasiojulikana.

Katika shambulio hilo ambalo limelaaniwa na watu wengi wa ndani na nje ya nchi, Lissu alivunjika mguu wa kulia, mkono wa kushoto na nyonga na ameshafanyiwa jumla ya operesheni 14 katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Dodoma na Hospitali ya Nairobi.

Baada ya tukio hilo, Lissu (49), aliwahishwa katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Dodoma ambako alipatiwa matibabu ya awali kabla ya kusafirishwa kwenda Kenya kwa ajili ya matibabu zaidi.

Taarifa za awali zilidai watu waliompiga risasi walikuwa wakimfuatilia kutoka bungeni, na kwamba walikuwa wakitumia gari nyeupe aina ya Nissan Patrol.

Hadi sasa polisi haijamkamata mtu yeyote kuhusiana na shambulio hilo la kinyama.

Post a Comment

Previous Post Next Post