TIMU ya taifa ya Nigeria imefuzu kushiriki Fainali za Kombe la Dunia mwakani baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Zambia katika mchezo wa Kundi B jana Uwanja wa Akwa Ibom mjini Uyo.
Shukrani kwake mfungaji wa bao hilo pekee linaloipeleka Nigeria Urusi mwakani, winga wa Arsenal, Alex Iwobi aliyewainua vitini mashabiki wa Super Eagles dakika ya 73 baada ya nyota wa Chelsea, Victor Moses kushirikiana vizuri na Abdullahi Shehu kumsetia mfungaji kumaliza kazi.
Tunisia nayo imejiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu baada ya ushindi wa 4-1 dhidi ya Guinea kwenye mchezo wa Kundi A, huku Youssef Msakni akipiga hat-trick na Mohamed Ben Amor akifunga lingine.
Naby Keita aliwafungia Guinea dakika ya 35 kabla ya kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya mwisho.
Tunisia inaongoza Kundi hilo kwa pointi tatu zaidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo walioshinda 2-1 dhidi ya Libya jana kuelekea mechi za mwisho.
Misri wanaweza kuwa timu nyingine kujihakikishia tiketi mapema kama wataifunga Kongo leo baada ya jana Uganda kulazimishwa sare ya 0-0 na Ghana katika mchezo wa Kundi E mjini Kampala.
Katika Kundi A, Tunisia imeshinda 4-1 dhidi ya Guinea na watafuzu Kombe la Dunia watatoa sare nyumbani na Libya Novemba. Wakifungwa, DRC itafuzu ikiifunga Guinea.
Kundi B Nigeria imejihakikishia kwenda Urusi baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Zambia jana.
Kundi la kifo ni C, ambalo kwa sasa Morocco wanaongoza baada ya kuichapa Gabon 3-0. Nchi hiyo ya Kaskazini mwa Afrika sasa itatakiwa kuepuka kufungwa na Ivory Coast, vinginevyo Tembo watafuzu badala yao.
Senegal wanaongoza Kundi D kwa pointi mbili zaidi huku wakiwa na mchezo mmoja mkononi. Wakishinda dhidi ya Afrika Kusini watakwenda Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu 2002 walipokwenda kwa mara ya kwanza na kufika Robo Fainali.
Kundi E baada ya sare ya 0-0 baina ya wenyeji Uganda na Ghana, leo Misri wanaikaribisha Kongo.
Hivyo ndivyo mambo yalivyo kwa Afrika kufuzu Kombe la Dunia
Post a Comment