Mwalimu wa madrasa, Abdillah Sharifu, amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela baada ya kutiwa hatiani kwa kumlawiti mtoto wa kiume wa miaka 11.
Sharifu (30), mkazi wa Gongo la Mboto eneo la Moshi Baa amehukumiwa kifungo leo Jumanne katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala.
Mshtakiwa anadaiwa kumlawiti mtoto huyo na pia kumtishia kuwa angemroga endapo angetoa taarifa kwa wazazi wake kuwa anamfanyia kitendo hicho.
Akisoma hukumu, Hakimu Mkazi Mwandamizi, Juma Hassan amesema ameridhishwa na ushahidi wa mashahidi wanne akiwemo daktari.
"Mshtakiwa nimekutia hatiani kama ulivyoshtakiwa, ninakuhukumu kifungo cha miaka 30 jela ili iwe fundisho kwako na watu wengine wenye tabia mbaya kama hii," amesema.
Hakimu Hassan amesema kitendo kilichofanywa na mshtakiwa ambaye ni mwalimu wa dini ni cha kikatili.
Akipitia ushahidi wa upande wa mashtaka, hakimu Hassan amesema shahidi wa kwanza ambaye ni mtoto huyo aliieleza Mahakama kuwa mshtakiwa Februari 25 alimtaka kwenda nyumbani kwake.
Baada ya kufika nyumbani kwa mshtakiwa ambaye mke wake ana tatizo la kutoona, shahidi huyo alieleza alitakiwa kuvua nguo kitendo ambacho pia kilifanywa na Sharifu.
Shahidi huyo aliieleza Mahakama kuwa mshtakiwa alimfanyia ukatili huo, huku akimtishia kuwa iwapo angethubutu kutoa siri hiyo angemroga.
“Mara kwa mara alikuwa akinifanyia mchezo huu hadi nilipomwambia mama na kisha kwenda kufungua kesi katika kituo cha polisi Mazizini,” alisema mtoto huyo katika ushahidi alioutoa mahakamani.
Katika ushahidi wa mama mzazi wa mtoto huyo, alidai baada ya kuripoti polisi walikwenda hospitali ambako kwa mujibu wa vipimo vya daktari licha ya kutokuwa na michubuko ilionekana aliingiliwa.
Mshtakiwa alidai ana mke kipofu na kwamba, hafanyi vitendo hivyo isipokuwa alikuwa na ugomvi na mama wa mtoto huyo na ndiyo sababu ya kumfungulia kesi.
Hata hivyo, mshtakiwa alishindwa kuifafanulia Mahakama chanzo cha ugomvi hivyo ilitupilia mbali utetezi wake na kumtia hatiani.
Awali, Wakili wa Serikali, Grace Mwanga aliiomba Mahakama kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia za kulawiti watoto na wanaotumia kimvuli cha nyumba za ibada kufanya ukatili.
Mshtakiwa alitenda kosa hilo, Februari 25 katika eneo la Moshi Baa, Gongo la Mboto.
Post a Comment