Matumizi ya Mkaa husababisha Uharibifu wa Misitu


Taarifa za wataalamu wa misitu zinaonyesha kuwa uharibifu wa misitu kutokana na matumizi ya mkaa ni hekta 372,000 kwa mwaka.

Kiwango hicho ni sawa na asilimia 1.1 ya eneo lote lenye miti na katika Jiji la Dar es Salaam pekee zaidi ya magunia 500,000 ya mkaa huingizwa kila mwezi.

Uvunaji na usafirishaji haramu na holela wa mazao ya misitu hususan mkaa kwa kutumia pikipiki na baiskeli ndani ya misitu ya hifadhi, mapori ya akiba na hata ndani ya hifadhi za Taifa unatajwa kuwa chanzo kikuu cha baa hili.

Inaelezwa kuwa pikipiki 20 zikisafirisha mkaa ni sawa na lori moja lililojaa mkaa. Aidha, njia hii ya usafirishaji inachangia ukwepaji wa makusanyo ya maduhuli ya Serikali.

Kufuatia changamoto mbalimbali za usafirishaji wa mazao ya misitu nchini Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) mwaka huu iliunda kikosi kazi kwa kushirikisha Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) na Kikosi cha Usalama Barabarani  ili kutekeleza sheria na kanuni za usafirishaji wa mazao ya misitu.

Kikosi kazi hicho kinalenga kudhibiti usafirishaji wa mazao ya misitu kwa baiskeli na pikipiki katika barabara za mikoa ya Dar es Salaam, Iringa, Morogoro na Pwani.

Mkurugenzi wa mipango na matumizi endelevu ya misitu na nyuki nchini, Mohamed Kilongo anasema TFS imekuwa ikitoa elimu inayohusu usafirishaji wa mazao ya misitu hususan mkaa baada ya kubaini kuwa ndio kichocheo kikubwa cha uharibifu wa mazingira.

Anasema mazao ya misitu huvunwa kinyume na taratibu na kusafirishwa kwa kutumia pikipiki na baiskeli, jambo ambalo pia ni kinyume na sheria.

“Usafirishaji wa mazao ya misitu kwa baiskeli na pikipiki unakiuka Mwongozo wa Uvunaji Endelevu wa Mazao ya Misitu, 2015 unaoeleza kuwa vyombo vya usafiri vinavyoruhusiwa kusafirisha mazao ya misitu ni vile vyenye magurudumu manne,” anasema Kilongo.

Anasema mwongozo huo ulizingatia pia sheria nyingine za nchi zikiwemo Sheria za Usalama wa Barabarani na Sumatra, lakini pia kubana mianya ya wizi na ukwepaji mkono wa sheria za usimamizi wa maliasili nchini.

“Kwa upande wa Sumatra kupitia Kanuni ya Leseni za Usafirishaji ya Mwaka 2010, inatambua pikipiki kama chombo cha kusafirisha abiria na si vinginevyo na Sheria ya Usalama Barabarani Sura Namba 168 iliyorejewa mwaka 2002 inatambua pikipiki na baiskeli kama chombo cha usafirishaji kwa ajili ya abiria na si mizigo,” anasema mkurugenzi huyo.

Aidha, anasema kwa mujibu wa tathmini iliyofanyika Novemba mwaka jana hadi Januari mwaka huu, katika barabara kuu za Bagamoyo, Kisarawe, Morogoro na Kilwa zinazoingia jijini Dar es Salaam, jumla ya pikipiki 582 zimebainika kubeba mazao ya misitu kinyume cha sheria kila siku.

Hata hivyo, katika eneo la Visakazi katika Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze kunaonekana kuwa na usafirishaji hatari zaidi wa mazao ya misitu kwa kutimia pikipiki.

Baadhi ya wakazi wa eneo hilo wanaeleza kuwa, biashara ya mkaa imekithiri kwa sababu ndiyo njia pekee ya kuwapatia kipato na usafirishaji wa mazao ya misitu kutoka maeneo mbalimbali ni ajira inayowaingizia kipato.

“Tunalazimika kusafirisha kwa njia ya pikipiki na baiskeli kwa kuwa mtaji wetu mdogo na hivyo tunashindwa kumudu gharama za kukodi magari kwa shughuli hiyo,” anasema mfanyabiashara wa mkaa pembezoni mwa barabara aliyejitambulisha kwa jina la mama Khadija.

Anayataja maeneo maarufu ya uvunaji wa mazao ya misitu hususan mkaa kuwa ni pamoja na Lukwambe, Mkono wa Tembo, Ubena na Chamlugwa yote ya wilayani Chalinze.

Ukwepaji makusanyo ya Serikali

Kuhusu ukwepaji wa makusanyo ya maduhuli ya Serikali, Khadija anasema wanalipa ushuru wa Serikali ya kijiji pamoja na halmashauri, lakini hawamudu kulipa ushuru wa Wakala wa Huduma za Misitu kwa kuwa gharama zake ni kubwa.

Anasema wamekuwa wakilipa ushuru wa kijiji wa Sh500 kwa gunia moja kwenye vijiji wanavyovuna na wanapoufikisha pembezoni mwa barabara mteja anayenunua mkaa anawajibika kulipa ushuru wa halmashauri wa Sh1,800 kupitia wakala wa ushuru wa halmashauri.

Ofisa wa Wakala wa Ushuru wa halmashauri hiyo, Afrikanus Silvanus anakiri kuwa wafanyabiashara wa Visakazi hufanya biashara na kusafirisha mazao ya misitu kwa nyakati zote, mchana na usiku.

Anasema kuwa yeye binafsi hupokea ushuru wa halmashauri hadi nyakati za usiku, pale ambapo kuna uhitaji jambo ambalo ni kinyume na sheria.

DC alia usimamizi wa sheria

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema ni miongoni mwa watu walioshuhudia usafirishaji wa mazao ya misitu kwa njia ya pikipiki anasikitika kuona sheria zipo na wanaozisimamia wapo, lakini hawatekelezi wajibu wao hali inayosababisha misitu kuendelea kuteketea.

“Inawezekanaje vyombo vinavyosafirisha mazao ya misitu kinyume na sheria, hususan baiskeli na pikipiki vinapita mbele ya askari wa usalama barabarani na hachukuliwi hatua? Inawezekanaje hawa wanapita na magunia yenye uzito zaidi ya unaostahili?” anahoji Mjema na kuongeza:

“Inawezekana vipi halmashauri inaukatia ushuru mzigo huo? Inawezekanaje anapita kwenye vizuizi vyenye watu wa usalama baada ya giza kuingia ili hali hairuhusiwi? Kila mtu na atimize wajibu wake misitu yetu itapona.”

Mei 26, 2016 Wizara ya Maliasili na Utalii na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) walisaini makubaliano kuimarisha ushirikiano katika usimamizi wa misitu kwa pamoja, malengo ambayo kila upande  ukitekeleza majukumu yake kama yalivyoainishwa katika makubalino hayo usimamizi endelevu wa  misitu    utaimarika  kwa faida ya Taifa.

RC Ndikilo atoa agizo

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo akifungua mkutano wa siku moja wa Kanda ya Mashariki kuhusu utekelezaji wa randama ya makubaliano ulioandaliwa na TFS na kufanyika katika ukumbi wa Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (Tafori) mjini Morogoro wiki iliyopita alisema kwa kuzingatia umuhimu wa hifadhi za misitu, ni vyema kila mwananchi akazingatia maagizo ya Serikali.

Ndikilo anawataka wananchi kufuata sheria za nchi zinazohusiana na uhifadhi wa maliasili na kuachana na tabia ya uharibifu wa miti kwa kuwa huko ni kuhatarisha vizazi vilivyopo na vijavyo.

“Naagiza, wale wote wanaofanya biashara ya mkaa kuzingatia sheria na taratibu ikiwamo uzito wa gunia la mkaa uliowekwa (kilo 50). Ni marufuku mazao ya misitu kusafirishwa na vyombo visivyoruhusiwa kisheria, hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakaesafirisha, kununua au kuuza mazao yaliyovunwa kinyume na sheria,”anasema.

Anaongeza kuwa zaidi ya asilimia 70 ya mkaa unaozalishwa mikoani huingia Dar es Salaam kwa njia zisizo halali kama vile magari yaliyofunikwa, baiskeli na pikipiki, na endapo hatua madhubuti za kudhibiti uharibifu huo hazitachuliwa haraka nchi itakuwa jangwa siku za karibuni..

Post a Comment

أحدث أقدم