Serikali imesema baadhi ya vifaa tiba vya matibabu ya mionzi vitaanza kuzalishwa nchini baada ya kuingia makubaliano ya ushirikiano na Kampuni New Soft ya China.
Baadhi ya vifaa hivyo ni Ultrasound, CT-scan, MRI na Digital X-Ray.
Hata hivyo, Serikali haikueleza uzalishaji huo utaanza lini ambao umelenga kuboresha huduma kwa Watanzania.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo, Jinsia ya Watoto na Wazee, Dk Faustine Ndugulile alitoa kauli hiyo jana katika hotuba yake iliyosomwa na James Boyi ambaye pia ni Mkuu wa Huduma za Radiolojia kutoka wizara hiyo.
Dk Ndugulile alieleza hayo wakati akifungua mkutano wa Chama cha Wateknolojia wa Matumizi ya Mionzi katika Uchunguzi na Tiba ya Magonjwa (Tara), uliokwenda sambamba na kuadhimisha siku ya 122 kimataifa ya ugunduzi wa mionzi duniani.
“Vifaa hivi vitakuwa vikizalishwa hapa hapa. Pia wataalamu watapata fursa ya kupewa mafunzo ya utengenezaji na uendeshaji wa vifaa hivyo nchini,” alisema Dk Ndugulile.
Awali, mwenyekiti wa Tara, Stephen Mkoloma aliwahikikisha Watanzania kuwa mionzi ya hospitali ni salama na aliwataka kujitokeza mapema kwa ajili ya uchunguzi na wakigundulika wana matatizo waanze matibabu haraka.
“Mfano kama una tatizo la saratani nenda hospitali usiende kwa mganga wa kienyeji, hakuna mganga wa kienyeji anayeweza kutibu saratani. Pia hakuna utafiti uliofanyika kwamba mtu ametumia dawa za kienyeji amepona,” alisema.
Mkoloma alifafanua kuwa wao kama wataalamu wapo tayari kuwahudumia Watanzania huku akisisitiza kuona umuhimu wa kwenda hospitali kwa ajili ya kufanya uchunguzi dhidi ya afya zao
By nandondeblogspot.
إرسال تعليق