Hizi ndio sababu DED Butiama kutumbuliwa



RAIS John Magufuli, ametengua uteuzi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama mkoani Mara, Solomoni Ngiliule, kutokana na makosa ya ubadhirifu wa fedha za umma.

Taarifa ya kutenguliwa huko ilitolewa jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi), Selemani Jafo, alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Jafo alisema Rais Magufuli ametengua uteuzi wa Mkurugenzi huyo kuanzia jana na kwamba uchunguzi zaidi unaendelea ili kubaini ubadhirifu huo ni wa fedha kiasi gani.

Alisema ubadhirifu huo umefanywa kwenye fedha za miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwamo miradi ya maji.

"Hatua hiyo imetokana na ziara ya kikazi aliyoifanya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, mkoani Mara na kubaini baadhi ya watendaji kwenye mamlaka za serikali za mitaa wameshindwa kutimiza majukumu yao ambayo wamepewa dhamana ya kuwatumikia wananchi," alisema.

Alisema kutokana na ziara hiyo ya Waziri Mkuu, Rais Magufuli amefikia hatua ya kutengua uteuzi huo kwani Mkurugenzi huyo ameshindwa kutimiza majukumu yake kama Mkurugenzi mwenye dhamana na kusababisha ubadhirifu wa fedha za umma.

Jafo alimwagiza Katibu Mkuu Tamisemi kumchukulia hatua stahiki Mweka Hazina wa halmashauri hiyo kutokana na matumizi mabaya aliyoyafanya ya fedha za serikali.

"Hatua zichukuliwe kwa mweka hazina ambaye kipindi ambacho ubadhirifu huo ulitokea akiwa madarakani," alisema.

Aidha, Waziri Jafo aliwataka watumishi wote walioko kwenye mamlaka za serikali za mitaa kufanya kazi kwa weledi na kuzingatia kanuni za utumishi wa umma na kuhakikisha rasilimali fedha za nchi zinatumika kwa maslahi mapana ya Taifa.

"Watendaji wa mamlaka za serikali za mitaa acheni kufanya kazi kwa mazoea kwa kuwa kutenguliwa kwa wakurugenzi siyo mara ya kwanza, suala hilo limekuwa likijirudia kutokana na kufanya kazi kwa mazoea na kukosa uadilifu," alisema.

Wakurugenzi wengine waliowahi kutenguliwa uteuzi kutokana na tuhuma mbalimbali ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya mji Tunduma na Halmashauri ya Nkasi.

Januari 20, mwaka huu, Majaliwa alifanya ziara katika Wilaya ya Butiama na kumuagiza Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Raphael Nyanda, kutuma timu ya wakaguzi kwenda kufanya ukaguzi maalum katika ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo.

 Majaliwa alisema halmashauri hiyo imekuwa na tabia ya kutumia fedha za miradi mbalimbali ya maendeleo zinazotolewa na Serikali katika shughuli nyingine, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Majaliwa akizungumza na watumishi na madiwani wa halmashauri hiyo, aliagiza kuchunguzwa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Mweka Hazina wa Halmashauri Masanja Sabuni na Ofisa Manunuzi wa Halmashauri  hiyo Robert Makendo.

Alisema viongozi hao wanatakiwa wachunguzwe kutokana na matumizi yasiyoeleweka ya fedha za miradi ya maendeleo zinazotolewa na Serikali zikiwamo Sh. milioni 12 walizotumia kuandaa wasifu (profile) ya Halmashauri hiyo.

Waziri Mkuu alisema fedha zingine ni pamoja na Sh. milioni 70 za elimu maalum, Sh. milioni 288 za mradi wa maji Butiama ambazo zote hazijulikani zimetumikaje.

"Hatuwezi kuvumilia vitendo hivi, fanyeni uchunguzi na naomba taarifa yake mara mtakapokamilisha," aliagiza Majaliwa

Post a Comment

أحدث أقدم