Dar es Salaam. Sheria za kimila zimetajwa kama moja ya kikwazo kwa wanawake kumiliki ardhi licha ya Sheria za nchi kuzingatia usawa wa kijinsia.
Hoja hiyo imetolewa leo Agosti 24,kwenye Mkutano wa pili wa wadau wa kutetea haki na asasi za kiraia unaoendeshwa na Shirika la Oxfam Tanzania pamoja na Jukwaa la ardhi(TALA) juu ya haki ya mwanamke kumiliki ardhi.
Mwanasheria wa Kituo cha Msaada wa Sheria kwa wanawake(WLCA) Wigayi Kissandu amesema Sheria ya ardhi ya mwaka 1999 inatoa haki sawa lakini inakinzana na Sheria za kimila.
"Sheria inampa haki mwanamke kumiliki ardhi lakini inakumbana na kizingiti kingine kwenye sheria ya ardhi ya kimila inayomnyima haki ya kurithi ardhi kutoka kwa familia,” amesema.
Mkuu wa Kitengo cha Ushawishi na Utetezi wa Oxfam Tanzania, Eluka Kibona amesema tatizo kubwa ni mfumo dume unaomzuia mwanamke kumiliki ardhi.
Majadiliano hayo yamelenga kuhamasisha kutambulika kwa haki za ardhi hasa kwa wanawake kwa kuwashirikisha wadau ikiwamo Wizara ya ardhi, Katiba na Sheria pamoja na wadau wa maendeleo.
Pia, Mkutano huo utasaidia kuboresha Kampeni ya "Wanawake na ardhi" itakayoanzishwa hivi karibuni
Post a Comment