Wafanyakazi wa Bank wapigwa marufuku kutumia simu za mkononi wakiwa Kazini


MKURUGENZI Mtendaji wa Taasisi ya Mabenki Tanzania (TIOB), Patrick Mususa amesema matumizi ya simu binafsi za mkononi yanayofanywa na baadhi ya wafanyakazi wa mabenki wakati wa kazi, yanapaswa kudhibitiwa. Badala yake amesema, simu za mezani za ofisi zitumike wakati wote wa kazi wanapowahudumia wateja.

Kutokana na baadhi ya wafanyakazi wa benki kuhusishwa na uhalifu wa kushambuliwa kwa risasi na kisha kuporwa fedha na majambazi kwa baadhi ya wateja wao, mkurugenzi huyo wa TIOB amesema matumizi ya simu binafsi kwa wafanyakazi wa benki yanatakiwa kufanyika nje ya eneo la benki baada ya kazi. “Zitumike simu za ofisi wakati wa kazi tena kwa matumizi ya kiofisi ikiwemo kuwahudumia wateja wao.

Mteja anaweza kuruhusiwa kutumia simu yake ndani ya benki pale tu anapotakiwa kufanya muamala na benki husika,” alieleza Mususa alipozungumza na gazeti hili. Mususa alisema taasisi yake inahusika na kutoa masomo ya kitaaluma ya mwaka mmoja kwa wafanyakazi wa mabenki ili kuwajenga kitaaluma na kimaadili. Alisema TIOB inawasaidia wenye mabenki kupata wafanyakazi wanaojua uzito na umuhimu wa majukumu wanayopewa wakati wanapowahudumia wateja wao.

Alisema kati ya wanachama 7,000 wa TIOB, wanachama wenye vyeti vya taasisi hiyo vinavyowapa sifa ya kufanya kazi kwenye mabenki hawazidi 600. Mususa aliongeza kuwa changamoto iliyopo ni kwa baadhi ya wamiliki wa mabenki nchini kuajiri watu wanaohitimu vyuo bila kupitia TIOB ili wapikwe kimaadili.“Kwa mfanyakazi ambaye ni mwanachama wetu, ikiwa atathibitika kujihusisha na vitendo vya uhalifu kama huo, kwanza tunamfukuza uanachama na kisha tunakibatilisha cheti chake cha kitaaluma tulichompatia na hawezi kuajiriwa mahali pengine, hivyo tunawashauri wenye mabenki wanapoajiri wafanyakazi wapya wawalete TIOB,” alieleza.

Kwa upande wao, Chama cha Wamiliki wa Mabenki Tanzania (TBA), kimesema hakina taarifa rasmi kuhusu wahudumu wa benki kuhusika kwenye uhalifu wa kuporwa fedha kwa wateja wanaowahudumia. Akizungumza na gazeti hili mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi Mtendaji wa TBA, Tusekelege Joune alisema hawajawahi kupata kesi au taarifa rasmi inayowahusisha wahudumu hao wa benki kushirikiana na majambazi wanaowavamia na kuwapora fedha wateja wanapotoka benki.

Joune alisema baadhi ya wafanyakazi wa benki mara nyingine huwa wanahusishwa na baadhi ya uhalifu unaotokea ndani ya benki, lakini hawajawahi kusikia wahudumu hao kutuma ujumbe kwa majambazi kupitia simu zao za mkononi kwa sababu taratibu za kazi haziwaruhusu kutumia simu hizo na mfanyakazi anapobainika kufanya hivyo anapaswa kuchukuliwa hatua za kinadhimu na benki husika.

Wakati TBA wakisema hawana taarifa rasmi ya baadhi ya wahudumu wa benki kujihusisha na uhalifu wa kuporwa fedha kwa wateja, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alinukuliwa na gazeti hili Septemba 14, mwaka huu akiwaambia waandishi wa habari kwamba watu wawili wanashikiliwa na polisi baada ya Meja Jenerali mstaafu, Vincent Mribata kushambuliwa kwa risasi na majambazi Septemba 11, 2017 wakati anaingia getini nyumbani kwake Tegeta jijini Dar es Salaam na kuporwa kiasi cha Sh milioni tano.

Kamanda Mambosasa aliwataja watu hao kuwa ni Godfrey Gasper ambaye ni mlinzi wa nyumba ya Meja Jenerali Mribata pamoja na mfanyakazi wa Benki ya NBC tawi la Tangibovu katika Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam. Joune alieleza kuwa wao kama TBA hawana uwezo wa kumwadhibu moja kwa moja mhudumu wa benki anayethibitika kuhusika na uhalifu huo, ila kinachofanyika ni benki husika kutoa taarifa kwao baada ya kumwadhibu ili taarifa hizo zihifadhiwe kwenye tanzidata zao kwa kumbukumbu.

Aidha, alisema polisi waliwahi kufanya utafiti na kubaini kuwa wanaohusika kutoa taarifa za wateja siyo wafanyakazi wa benki, bali ni watu wanaojifanya wateja wanaoingia ndani ya benki wakiwa na lengo la kufuatilia ni mteja yupi anachukua fedha nyngi. “Polisi waliwahi kufanya utafiti kuhusiana na matukio kama haya miaka miwili iliyopita na walitualika wakati wanafanya uwasilisho (presentation) wao. Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai wakati huo (DCI) Diwani Athumani alikuwepo.

“Polisi walieleza kwenye taarifa yao kuwa wanaotoa taarifa hizo siyo wafanyakazi wa benki, bali ni baadhi ya watu wanaojifanya wateja ambao hufuatilia kwa kuangalia kiasi gani cha fedha mteja anajaza kwenye fomu zao kwa kuchungulia kwa karibu na mara nyingine hujifanya kuomba peni au msaada kutoka kwa wateja hao, lakini lengo lao ni kuona kiasi cha fedha ambacho mtu anataka kutoa,” alieleza Joune.

Aliongeza kuwa kwa mujibu wa utafiti huo wa polisi, watu hao ndiyo hutoa taarifa kwa wahalifu wenzao walio nje ya benki kwani wanakuwa wameshajua kiasi cha fedha ambacho mtu amechukua lakini pia na rangi ya nguo ambayo mteja amevaa kwa wakati huo. Ili kukabiliana na uhalifu huo, Mkurugenzi Mtendaji huyo wa TBA alisema wanalifanyia kazi suala hilo kwa karibu kwa kushirikiana na taasisi nyingine ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Polisi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa Makosa ya Jinai (DCI), Mahakama na Tume ya Sheria ili waje na mkakati wa pamoja wa kulidhibiti.

Alisema wateja hawana sababu ya kuhatarisha maisha yao kwa kutembea na fedha nyingi mifukoni au kwenye mabegi nyakati hizi ambazo teknolojia ya kufanya miamala imeboreshwa, badala yake ni vyema wakatumia kadi zao za benki za kielektroniki kufanya malipo ya ada, kununua magari, kununua vifaa vya ujenzi na manunuzi mengine.

Alisema TBA wako kwenye mchakato wa kuanzisha mfumo mpya wa malipo utakaoziunganisha benki zote ili kumpa mteja uhuru na urahisi wa kutuma fedha kutoka benki moja kwenda nyingine tofauti na ilivyo sasa ambako baadhi ya wateja kutokana na uharaka walionao wanalazimika kuhamisha fedha taslimu, jambo ambalo ni hatari kwa maisha yao.

Kwa mujibu wa Joune, mabenki yanaajiri wahitimu wa vyuo vikuu, lakini wahitimu waliopitia TIOB na wenye vyeti vya taasisi hiyo ndiyo wana nafasi kubwa ya kupata ajira. Alisema kwa awali wafanyakazi wa benki ambao hawakupitia kwenye taasisi hiyo kwa mafunzo zaidi ya kibenki, walikuwa hawapandishwi vyeo wala kupandishiwa mshahara. Alisema kwa sasa kuna mpango unaandaliwa ili iwe lazima kwa wafanyakazi wa benki kwenda kupata mafunzo zaidi ya kibenki TIOB.

Post a Comment

Previous Post Next Post