Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mhe Halima Dendego akizungumza na viongozi wote wa Mikoa ya Lindi na Mtwara juu ya kusimamia kikamilifu Mpango wa Kitaifa wa usajili na kuwapatia vyeti vya kuzaliwa watoto wote wenye umri chini ya miaka mitano, uliofanyika mkoani humo jana.
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mhe Halima Dendego amewaagiza viongozi wote wa Mkoa huo kujipanga na kusimamia kikamilifu Mpango wa Kitaifa wa usajili na kuwapatia vyeti vya kuzaliwa watoto wote wenye umri chini ya miaka mitano kwa kufikia lengo la asilimia mia moja ndani ya kipindi kifupi cha miezi mitatu.
Mhe Dendego ameyasema hayo hii leo Mkoani Mtwara alipokuwa akifungua mafunzo maalum yaliyoandaliwa na RITA kwa viongozi wa Mkoa kuhusu utekelezaji wa mpango huo na kuwaagiza viongozi wote kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa mpango huo kwa Taifa kwani utawezesha upatikanaji wa takwimu sahihi zitakazosaidia katika mipango ya maendeleo na kufahamu makundi mbalimbali katika utoaji wa huduma za elimu,afya pamoja na ajira.
Ameongeza kuwa, Takwimu za Vizazi ni kichocheo cha maendeleo nchini kwani Serikali huhitaji takwimu hizi kwa ajili ya kupanga mipango ya maendeleo ya muda mfupi na muda mrefu na kwamba mipango mingi ya serikali huanzia katika ngazi ya Halmashauri hivyo bila ya takwimu itakuwa vigumu kwa halmashauri kuweza kujua kwa usahihi mahitaji ya kupeleka huduma muhimu kwenye jamii.
“Kwa mfano ni muhimu kujua katika miaka mitano ijayo kutakuwa na wanafunzi wangapi wanaohitaji kuanza elimu ya msingi”. Amesema.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Lindi Mhe Shaibu Ndemanga kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa huo Mhe Godfrey Zambi, amesema mpango huo umeleta suluhisho la kudumu kwa Wananchi wanaoishi Vijijini ambao wamekuwa wakitumia gharama kubwa kufika makao Makuu ya Wilaya ili wapatiwe huduma hiyo.
Mhe Ndemanga ameongeza kuwa Mkoa wa Lindi umepokea kwa furaha na kuwahidi kutoa elimu zaidi kwa wananchi wake ili kuchangamkia fursa hiyo hasa ukizingatia umuhimu wa cheti cha kuzaliwa hasa kwa kipindi hiki ambapo ili Mwananchi aweze kupata huduma mbalimbali ni lazima atahitajika kuwasilisha nyaraka hiyo.
“tumeona wenzetu wa bima ya afya lazima uwe na cheti cha kuzaliwa cha mtoto na kwa sasa ili mtoto apate elimu itamlazimu awe na cheti cha kuzaliwa.
Naye Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA Bi Emmy Hudson amesema kuwa Katika Mpango huo watoto watasajiliwa na kupatiwa vyeti vya kuzaliwa hapo hapo bila malipo (bure) katika vitu vya Tiba vinavyotoa huduma ya mama na Mtoto pamoja na Ofisi za watendaji kata tofauti na utaratibu uliozoeleka hapo awali ambapo iliwabidi kwenda katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya.
Bi Hudson ameongeza kwamba serikali imesogeza huduma za usajili karibu na maeneo ya makazi ya wananchi hivyo kuwaondolea wananchi changamoto ya kusafiri umbali mrefu na kutumia gharama nyingi kuweza kupata huduma hii.
Tayari Mpango huu umeanza kutekelezwa katika Mikoa saba ya Mwanza, Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe, Geita na Shinyanga na kote umeonesha mafanikio chanya na kwa hivi sasa maandalizi yanaendelea kufanyikakwa ajili ya kuanza utekelezaji katika Mikoa ya Lindi na Mtwara.
Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA Bi Emmy Hudson akizungumza katika Mkutano na viongozi wote wa Mkoa mikoa ya Lindi na Mtwara juu ya kusimamia kikamilifu Mpango wa Kitaifa wa usajili na kuwapatia vyeti vya kuzaliwa watoto wote wenye umri chini ya miaka mitano, uliofanyika mkoani humo jana
Mkuu wa Wilaya ya Lindi Mhe Shaibu Ndemanga kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa huo Mhe Godfrey Zambi, akizungumza na viongozi wote wa Mikoa ya Lindi na Mtwara juu ya kusimamia kikamilifu Mpango wa Kitaifa wa usajili na kuwapatia vyeti vya kuzaliwa watoto wote wenye umri chini ya miaka mitano, uliofanyika mkoani humo jana .
Baadhi ya washiriki wa Mkutano huo.
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mhe Halima Dendego akiwa katika picha ya pamoja na menejimenti ya RITA.
إرسال تعليق